Featured

    Featured Posts

NGOSWE PENZI KITOVU CHA UZEMBE


UCHAMBUZI WA FASIHI SIMULIZI
KIPENGELE CHA FANI   NA MAUDHUI

MUHIMU KUZINGATIA:

mwanafunzi:  unatakiwa ufahamu vipengele vya fani na maudhui,  je  unavifahamu ???

je unafahamu ni kwa namna gani utaweza kukitumia kipengele cha fani kujibu maswali  endapo utahitajika kufanya hivyo ???

je unafahamu pia kupangilia insha yako ili iweze kuleta maana na yenye matumizi sahihi ya alama ???

je unafahamu kuwa ni rahisi mno kuchambua kazi ya fasihi kwa kutumia vitabu ??
muhimu zingatia
-mifano halisi ya wahusika
-mifano hiyo ihusiane na swali husika linavyouliuza
-mifano hiyo ihusiane  na mazingira halisi ya maisha ya jamii


kama ndivyo,    rejea  kusoma kwa makini kitabu hiki,na  kwa kuanza na kipengele cha fani   angalia namna  kitabu   kilivyochambuliwa:

*********ANZA*************  


JINA LA KITABU: NGOSWE PENZI KITOVU CHA UZEMBE
MWANDISHI: EDWIN SEMZABA
WACHAPISHAJI: NYAMBARI NYANGWINE PUBLISHERS
MWAKA: 2006

NGOSWE PENZI KITOVU CHA UZEMBE image

UTANGULIZI WA KITABU
Ngoswe penzi kitovu cha uzembe ni tamthiliya maarufu sana ambayo imewahi kuigizwa katika redio Tanzania na katika majukwaa mbalimbali hapa nchini. Ni tamthiliya ambayo imeundwa vyema katika vipengele vya fani na maudhui. Ameteua lugha nzuri na yenye mvuto kwa wasomaji yenye mbinu za kifasihi zilizosheheni, muundo wenye mtiririko mzuri, unaoakisi kuanza kuchipuka kwa matukio mpaka kilele cha matukio. Wahusika wamebeba vyema uhusika wao mfano Ngoswe.
Ameibua dhamira kuhusu mambo yanayoigusa jamii ya leo kama vile uzembe, madhara ya ulevi, uzembe kazini, suala la matabaka kati ya mjini na vijijini. Mtazamo, falsafa na msimamo wake ni kulenga kuibadilisha jamii na kuleta maendeleo.

JINA LA KITABU
Jina la kitabu “Ngoswe penzi kitovu cha uzembe” ni jina ambalo limesawiri vyema yaliyomo ndani ya kitabu hicho, kwani Ngoswe ndio jina la mhusika mkuu anayebeba dhamira kuu ya tamthiliya. Pia penzi limeonekana kuwa ni kitovu cha uzembe kwani ndio yaliyopelekea kuteketezwa kwa karatasi za takwimu za sensa. Hivyo jina la kitabu si tu kwamba limesawiri yaliyomo katika kitabu bali pia katika jamii.
FANI
MTINDO
Mtindo alioutumia mwandishi ni dayalojia au majibizano. Mwandishi amepanga visa na masimulizi kwa kutumia majibizano ya wahusika.
  • Matumizi ya nafsi
Matumizi ya nafsi ya kwanza. Mwandishi ndiye ameyafafanua na kuelezea baadhi ya matukio. Katika karibu kurasa zote mwandishi ameonekana kuwa ndiye msimuliaji wa matukio.
Matumizi ya nafsi ya pili
Hapa watu wawili na zaidi wanajibizana. Tamthilya hii wahusika wanaojibizana kuibua dhamira na migogoro. Kuna majibizano baina ya mzee Mitomingi, Ngoswe na Mazoea nk.unaweza kupata mfano uk. wowote kwani ndio mtindo uliotawala.

MUUNDO
Muundo uliotumika ni muundo wa mojakwamoja au sahili. Kwani ameonesha tangu mwanzo wa mambo mpaka mwisho, anajenga visa vidogo mpaka visa vikuu au kileleni.
Amepanga visa na matukio yake katika maonesho matano. Kila kichwa kina maelezo yaliyojadiliwa katika onesho hilo.

KIJITO
Hapa yanaeleza jinsi mambo yanavyoanza. Jinsi Ngoswe anavyoingia kijijini anavyopokelewa na kuanza kufahamiana na wenyeji wake.

VIJITO
Hapa Ngoswe anaanza kufanya kazi iliyompeleka kijijini na tunaanza kuoneshwa changamoto anazokumbana nazo.

MTO
Ni mwendelezo wa matukio ya mwanzo hapa visa vinazidi kukua.

JITO
Hapa Ngoswe anakumbana na changamoto nyingi zaidi katika kazi yake. Na hapa anazidi kuanguka kwani anajiingiza katika mapenzi na msichana Mazoea, anaendekeza ulevi na kuharibu kazi kabisa.

BAHARINI
Hapa inaoneshwa mwisho wa mambo jinsi yalivyokuwa. Yanaonekana mahojiano baina ya Serikali na Ngoswe na Mitomingi juu ya uzembe uliofanyika wa kupoteza takwimu na hapa ndipo suluhisho linapotolewa juu ya matatizo hayo.

WAHUSIKA
NGOSWE
  • Kijana wa kiume umri kati yamiaka 20-25
  • Ameelimika na amestaarabika
  • Anatumwa na serikali kufanya sensa kijijini
  • Anajihusisha na mapenzi na msichana mazoea
  • Ni mlevi
  • Hana umakini katika kazi
  • Aliharibu kazi ya serikali
  • Hafai kuigwa na jamii
MAZOEA
  • Ni msichana mwenye umri kati ya miaka 18-20
  • Ni binti wa Mzee Ngengemkeni Mitomingi
  • Hana elimu na hajastaarabika
  • Ana nidhamu ya woga
  • Ana tama
  • Hana msimamo alikubali kuchukuliwa na Ngoswe hali akijua alishatolewa mahari
  • Hafai kuigwa na jamii
NGENGEMKENI MITOMINGI.
  • Ni balozi katika kijiji chake
  • Ni baba mzazi wa Mazoea
  • Ameoa ndoa ya mitara, ana wake wawili
  • Hajaelimika
  • Anashikilia mila na desturi za kale
  • Mlevi
  • Mkali sana
  • Anateketeza karatasi za takwimu.
MZEE JIMBI
  • Mwanakijiji
  • Hajaelimika kwani hajui hata umri wake
  • Ni mlevi
  • Ana wake wawili
  • Anashikilia ukale
MAMA MAZOEA
  • Mke mkubwa wa Mitomingi
  • Mama yake Mazoea
  • Mlezi wa familia
  • Hapewi nafasi ya kutoa maamuzi katika familia
MAMA INDA
  • Mke wa pili Mzee Mitomingi
  • Mama yake Huzuni
  • Hapewi nafasi ya kutoa maamuzi
  • Ni mlezi wa familia.

MANDHARI
Mandhari ya tamthiliya hii imechorwa katika mazingira ya kijijini. Mambo yanayoelezwa ni ya kijijini mfano kilimo, hali ya watu kimaisha, huduma duni sana za kijamii kama vile shule, umbali wa makazi toka nyumba moja hadi nyingine. Haya yanatudhihirishia vyema mandhari hiyo ambayo kwayo imeibua dhamira mbalimbali kama vile umaskini, ukosefu wa elimu, huduma duni za afya vijijini, masuala ya imani potofu nk.

MATUMIZI YA LUGHA
Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha fasaha na rahisi kueleweka kwa wasomaji. Pia kuna matumizi ya lugha nyingine mfano uk. 1 “bell bottom”
  • Matumizi ya semi.

Methali
Uk.22 “Penye nia pana njia”.
Uk.27 “Waona vyaelea vyaundwa.”

Misemo
Uk.14 “Akuwaniae ujovu haji kweupe”

Nahau
Uk.11 “hebu keti tutupe mawe pangoni” – tule chakula
Uk.7 “mbongo zimelala”- ana maarifa
Uk.14 “pombe na yeye ni pete na chanda”- anapenda pombe sana.

  • Matumizi ya tamathali za semi.
Tafsida
Uk.21 “Wala hajarudi, kama ingekuwa ni kujisaidia si angekuwa amekwishamaliza?”

Tashbiha
Uk.1 “vumbi jekundu kama ugoro wa subiana”
Uk.8 “sarawili yake miguuni kama kengele ya bomani”
Uk.17 “wanaondoka huku wakitazamwa kama vile mizuka”
                                        
Sitiari
Uk.7 Mama Mazoea : “kiziwi mkubwa wee!”
Uk.14 “pombe na yeye ni pete na chanda!”
Uk.26. “karatasi? za takwimu? Ndio wanyama gani hao?”

Mubaalagha
Uk.11 Mama Mazoea : “kupeleka chakula ndio umefanya makao!”
Mama mazoea : “Kujibu swali ndio ukachukua mwaka mzima!”

  • Mbinu nyingine za kisanaa

Mdokezo
Uk.22 Mazoea : “sijui….. siwezi….. namuogopa baba”
Uk.16 Ngoswe : “huyo mtoto wenu wa kwanza anaishi hapa au…..”

Takriri
Uk.9 “Mama Masikio! We Mama Masikio!”
Uk.13. “Hodi! Hodi!”
Uk.2 “karibu karibu”

Tashtiti
Uk.5 Ngoswe: “hivyo waitwa nani?”
Mazoea: “mie?”
Uk.22 Ngoswe: “mchumba? Kwani mchumba ni kitu gani?”
Uk.26 Mitomingi: “karatasi? Za takwimu? Ndio wanyama gani hao?
Hapa wahusika waliuliza maswali ambayo majibu yake waliyaelewa ila kutokana na kutaka kudhihirisha hasira, msisitizo nk. Ndio maana wametumia tashtiti.
                   
Onomatopea/tanakali sauti
Uk.7 Kifaruhande anacheka “Ha! ha! ha!
      
  • Ujenzi wa taswira
Mwandishi ametumia taswira ya mto kuelezea visa vyake. Sehemu ya kwanza ni sehemu ya kijito, kijito ni kimto kidigo mwandishi hapa  anaanza kueleza mambo yakiwa machanga kabisa ndio yanaanza.
Sehemu ya pili ni vijito. Huu ni muunganiko wa vijito vidogovidogo hapa mwandishi anaanza kueleza visa  vidogovidogo. Sehemu inayofuata ni sehemu ya Mto. Hii inaashiria mambo yameanza kuwa mazito, visa vinakua zaidi na Ngoswe anazidi kuingia katika changamoto kubwa zaidi.
Pia Jito ni taswira ambayo mwandishi  ameitumia kuashiria hatari zaidi mambo makubwa zaidi na hapa ndipo tunaona Ngoswe anaanguka kabisa katika kazi yake kwani Jito ni lenye maji mengi na yanayoenda kwa kasi hivyo huhitaji umakini mkubwa zaidi.
Mwisho sehemu ya Bahari ambapo hapa ndipo hatima ya mambo inaelezwa Ngoswe anazama na kupotea kabisa! Hafanikiwi kutoa takwimu kwani karatasi zilichomwa moto.






JOKA LA MDIM

                     UCHAMBUZI  WA  KAZI  YA  FASIHI  SIMULIZI 


                                         JOKA LA MDIM

KIPENGELE  CHA  FANI.


(maalum kwa wanafunzi wa sekondari kidato cha nne school & private candidate)

         ZINGATIA:

1. (katika uchambuzi huu mwanafunzi atatakiwa kufahamu muundo na mtindo wa kitabu pamoja na matumizi  ya lugha ili kujibu maswali yatayohusiana na kipengele hiki)

2. (matumiz,  ya lugha hujumuisha lugha za picha, misemo,nahau na tamathali za semi katika kuwakilisha kazi zao)

3. (kumbuka katika uchambuzi wa vitabu hutumika wakati uliopo(simple present) na hii  ni pale unaponukuu baadhi ya maneno katika kitabu)

4.( kuna namna ya kuandika utangulizi(introduction) wakati wa kujibu swali lolote linalohusiana na kitabu cha kuzingatia  ni kwamba swali linataka nini )   kwa  mfano angalia swali hili    "waandishi wengi wa vitabu wamekuwa wakiyaona mambo katika jamii na kuyakosoa ili jamii ibadilike, tumia riwaya mbili ulizosoma kudhihirisha hili"

1. je umefahamu swali linataka nini ? (ujumbe?, maudhui?,au migogoro?)
2.je ni kwa vipi ungeonyesha riwaya utazotumia ?
3. je utaanza na riwaya gani, na utamaliza na ipi ?
4.je utahitimisha vipi insha yako ?
5. je utatumia mifano(quotation)  unapotetea hoja zako?



MWANDISHI: ABDALLAH J. SAFARI
MCHAPISHAJI      : HUDA PUBLISHERS
MWAKA: 2007

JOKA LA MDIMU image

UTANGULIZI WA KITABU
Joka la mdimu ni riwaya iliyojengwa kwa visa tofautitofauti vinavojengana kukamilisha masimulizi. Ni riwaya inayosawiri au kuakisi mambo yaliyopita ya nyakati za nyuma ambapo kulikuwa na shida kama vile za mafuta ya petroli, Nguo, vyakula nk. Pamoja na hayo zipo pia dhamira au mawazo ambayo yanasawiri maisha ya Mtanzania wa leo kama vile masuala ya rushwa na uhujumu uchumi.
Kwa upande wa fani ni riwaya ambayo mwandishi amewaumba vyema wahusika wake kwa kuwavika uhalisia vyema, amepanga visa vyake na amejitahidi kutumia lugha yenye mvuto na vionjo vya kisanaa huku akiwaburudisha wasomaji  kwa mtindo wa kipekee.

JINA LAKITABU
Jina la kitabu limewekwa katika lugha ya picha, JOKA LA MDIMU ni nyoka anayeishi katika miti ya kijani. Nyoka huyu hupendelea kuishi katika miti ya Minyaa na Midimu inayofanana na rangi yake. Nyoka huyu awapo kwenye miti hiyo si rahisi kumtambua kutokana na rangi yake kufanana sana na miti hiyo. Hivyo ni nyoka hatari sana kwa binadamu.
Mwandishi anatumia taswira ya Joka la Mdimu kufananisha na viongozi ambao ni wananchi wenzetu, wanafanana na sisi, ni ndugu zetu damu yetu. Lakini ni hatari mno kwani hutugeuka na kuwa mafisadi, wala rushwa, hawatimizi majukumu yao, ni walaghai nk. Badala ya kusaidia wananchi wao hujali maslahi yao kwanza na hivyo kusababisha mifumo ya kiuchumi kuendelea kuwa migumu kwa wananchi na kupelekea kuongezeka kwa kiasi kikubwa cha watu walio maskini au hohehahe. Hivyo jina la kitabu linasawiri yaliyomo ndani ya kitabu na katika jamii.

FANI
MUUNDO
Riwaya ya Joka la Mdimu imetumia muundo changamani yaani kwa kiasi fulani ametumia rejea au rukia pia ametumia muundo sahili au msago.
Mfano ametumia muundo wa rejea katika sura ya Mindule ambapo anaanza kutueleza juu ya habari za Amani dereva wa taxi na adha anazopata kutokana na ukosefu wa mafuta na jinsi anavyoiendesha biashara yake hiyo. Lakini ndani ya sura hiyohiyo anaturudisha nyuma na kuanza kutuelezea namna Amani alivyopata kazi ya udereva Taxi na kutueleza juu ya mmiliki wa Taxi hiyo ambaye ni Shiraz Bhanj. Pia katika  sura ya Boko anatueleza juu ya Safari ya Tino kwenda kumuona mwanae mgonjwa uk.73 ila hatuelezi inavyoendelea lakini anarukia kisa kingine cha Brown Kwacha na sura ya Kwale halafu badae anaturudisha nyuma na kuendelea kutuelezea juu ya habari za kuuguliwa kwa Cheche na Tino anapofika kumuona katika sura ya Dakta Makwati. Pia ametumia muundo wa moja kwa moja katika sura zingine kwani ameyapanga matukio yake katika usahili bila kuruka.
Pia mwandishi amegawanya visa na mtukio katika sura kumi ambapo kila sura ameipa jina kwa kutumia majina ya wahusika.

Sura ya kwanza, MINDULE
Hapa mwandishi anatueleza kuhusu habari za Amani dereva Taxi, masaibu anayopata katika kazi yake kutokana na uhaba wa mafuta katika vituo vya mafuta.

Sura ya pili, TINO
Hapa tunaelezwa kuhusu maisha ya Tino na kazi anazofanya ya kuvuta kwama. Tunaambiwa kuhusu hali ngumu ya maisha ya Tino na wakazi wengine wa Sega, hapa tunaelezwa pia kuhusu masuala ya uongozi jinsi ulivyo mbovu na ugawanywaji mbovu wa vyanzo vya uchumi na bidhaa.

Sura ya tatu, JINJA MALONI
Katika sura hii tunaelezwa kuhusu maisha ya Jinja Maloni, hapa anaibua dhamira kama vile za uvamizi, uhalifu na mauaji pia anaendela kutueleza kuhusu hali ngumu ya maisha.

Sura ya nne SEGA
Maisha ya wakazi wa Sega yanaelezewa hapa jinsi yalivyo ya dhiki, pia tunaelezwa kuhusu Tino na mkewe maisha yao yalivyo na familia yao, anaibua dhamira ya mapenzi ya dhati na upendo kwa familia.

Sura ya tano, BOKO
Hapa tunaelezwa kuhusu adha ya usafiri kwa watu, shida ya mafuta, ubovu wa miuondmbinu kama vile barabara, vinasemwa hapa.

Sura ya sita, BROWN KWACHA
Sura hii inaeleza habari za Brown maisha yake na tabia zake, anaibua dhamira kama vile uhujumu uchumi, biashara za magendo, suala la kutowajibika kwa watumishi, suala la kukosekana kwa uaminifu katika ndoa na mapenzi ya pesa ambapo sifa zote hizi alizibeba Kwacha.

Sura ya saba, KWALE
Hapa yanaelezwa mambo kuhusu hifadhi ya Kwale, safari ya Brown na Leila kwenda kutembea kwale. Hapa yanatajwa mambo ya udhalimu wa kuharibu mali za umma (maliasili za taifa) mfano pembe za ndovu, vipusa pia mapenzi yasiyo ya kweli.

Sura ya nane, DAKTA MIKWALA
Dakta Mikwala ndiye mhusika mkuu anayeelezwa hapa, tunalezwa juu ya ugumu wa upatikanaji wa huduma za afya kwani Cheche anashindwa kutibiwa kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni.

Sura ya tisa, CHECHE
Tunaelezwa juu ya juhudi za Amani na Tino ili kumsaidia Cheche aweze kwenda kutibiwa Uingereza. Wanafanikiwa kupora benki na kupata pesa za kumtibu Cheche.

Sura ya kumi, MOTO
Hapa hatma ya visa vidogo vidogo imeelezwa kwa kutolewa hatma ya maisha ya Cheche na Brown Kwacha. Cheche alipata matibabu na kupona na Browna anafanikiwa kuirubuni serikali kwa kuipanga mahesabu ya uongo.

MTINDO
Mwandishi ametumia mitindo ya aina tofautitofauti ili kuweza kuipamba kazi yake ivutie.
  • Matumizi ya nafsi.
  • Matumizi ya nafsi ya tatu Umoja. Imetawala.
Mfano uk.5 “Amani aliangalia…….” Uk.25 “Amani alijizuia” .
Nafsi ya tatuwingi; mfano uk. 63 “ wote walitoka nje kuelekea klabuni”.
Pia uk.53 “wale wanaume walimvamia”
  • Matumizi ya nafsi ya pili.
Mfano uk.106 “ mmechoka kuangalia video?” “aa tumeshaziona mara nyingi tunaomba aina nyingine.” Mazungumzo baina ya mke wa Brown na wanae.
Pia mazungumzo baina ya Brown na Leila.
Uk.113. “habari za asubuhi”
“ Nzuri sijui wewe” alijibu
“Uliota njozi njema?” 
"Wapi?"
"Kwa nini?"
  • Matumizi ya nafsi ya kwanza.
Mfano uk. 39 “mimi nimemaliza” “….kuiba nimeiba sana….”
  • Matumizi ya nyimbo. Uk.70. wimbo wa Chaupele
“Chaupele mpenzi, haya usemayo
Kama ni maradhi, yapeleke kwa Daktari
Wanambia niache rumba, na mimi sikuzoea
Sitaweza kuliacha rumba, kwa sababu yako
Kama wanipenda, nenda kwa baba”
Pia uk.58 “sega! Sega! Sega!, usioogope” wimbo waliouimba washabiki wa michezo.

  • Masimulizi ya hadithi ndani ya hadithi.
Hapa mwandishi amemtumia muhusika kusimulia kisa kingine kidogo ndani ya kisa kikuu. Mfano uk.39mhusika Tino anamsimulia mteja wake maisha yake ya mwanzo kabla hajaanza kazi ya kuvuta kwama.

MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi A. Safari ametumia lugha fasaha na inayoeleweka kwa wasomaji wake. Kuna matumizi ya lugha nyinginezo kama vile kiingereza. Uk.55 “city devils” uk.155 “I miss my family”, uk.24 “Hey man you will pay extra money”, uk.99 consignment”. Pia kuna matumizi ya lugha ya kiarabu, mfano uk.45 “Salaam aleikum mayitun” uk.42 “Inna Ilayhi Raajiunna!”, uk.13, “Insha Allah!”. Vilevile kuna matumizi ya lugha ya mtaani uk.39 “msela”, “ndito”, “kashkash”.
  • Matumizi ya tamathali za semi.
Tashibiha
Uk.117 “ngozi yake nyeusi kama udongo wa mfinyanzi”
Uk.122 “mweusi kama sizi la chungu”
Uk.9 “Zepher 6 ile iliunguruma kama simba dume”
Uk.10 “mteuzi mithili ya Mbega”
Uk.35 “……miguu yake ikakazana mithili ya upinde uliotaka kufyatuliwa”

Sitiari
Uk.91 “Brown Kwacha alikuwa kinyonga”
Uk.15 “sarahange wetu mboga kweli siku hizi”
Uk.40 “huku twakaa vinyama vya mwitu”
Uk.72 “sote ni kobe”
            Tashihisi
             Uk.109 “……gari lile zuri lilioondoka kwa madaha”
             Uk.143 “ kuta nyeusi za nyumba zaidi ya kumi zilisimama twe!kuomboleza”
              Uk.91 “pua zake zikalakiwa na riha na ashrafu ya manukato”
              Uk.12 “utumbo ulimlaumu”
              Uk.27 “mvua ikapiga kwa kiburi na kuviadhibu vibati vibovu”.
             
               Tafsida
              Uk. 49 “isijekuwa nimekukatiza haja!”, pia uk. hohuo “kinyesi”.
  • Mbinu nyingine za kisanaa.

         Takriri
            Uk.151 “mwizi! Mwizi! Jambazi! Jambazi!”
           Uk.57 “shinda! Shinda! Shinda!”
          Uk.33 “karibu baba, kariibu kaka, karibu mkwe”
         Uk.72 “uhuru upi? Uhuru gani? Uhuru wa nini na nani?”
         
     Mdokezo
        Uk.149 “lakini……..”
       
       Onomatopea au tanakali sauti
        Uk. 1 “saa mezani niliendelea kugonga taratibu ta! ta! ta!”
        Uk.10 “ikatoka sauti kali tupu ta nye nye”
        Uk.67 “upepo wa stova uliolia shshsh”
       
       Tashtiti
       Uk.113. leila anamuuliza Brown maswali ambayo anayajua majibu yake.
     Brown: “uliota njozi njema?
     Leila: Wapi?”
     Leila: Kwanini?
     Brown: Mwenywe unajua”
   
     Nidaa
     Uk.39 “Aaa! Limbukeni wa jiji anataka kunitia kashkash”
     Uk 30 “nguo zangu Mungu wee!”
    Uk.42 “Inna Lillah wa Inna Ilayhi Raajiunna!”
    Uk.92 “Ah! Leila kwacha alimsalimia kwa furaha”
   Uk. 105 “Lahaula”
  • Matumizi ya Semi.

Methali
Uk.78 “asilojua mtu ni usiku wa kiza”
Uk.83 “ukiona mwenzako anyolewa zako tia maji”
Uk.98 “mtaka waridi sharti avumilie miiba”
Uk. 99 “biashara haigombi”
Uk.43 “ajizi nuksani huzaa mwana kisirani”

Misemo
Uk.10 “asiye na bahati habahatishi”
Uk.47. “asiyezika hazikwi”
Uk.64 “mmetupa Jongoo na mtiwe”
Uk.98 “asali haichomvwi umoja”
Uk.111 “ajali haina kinga”
Uk.115 “mwenye macho haambiwi tazama”
Uk.120 “matendo hushinda maneno”
Uk.47. “asiyezika hazikwi”

Nahau
Uk.11 “sio unanilalia kila mara” – kunidhulumu
Uk.107 “alikonda akajipa moyo” – kujifariji moyo

  • Matumizi ya taswira
Taswira mwonekano imetumika, ambayo inatujengea picha kutokana na vitu tunavyovifahamu. Mfanouk.76 “alisema kijana mmoja wa kiume kavaa sketi, blauzi na sidiria iliyopachikwa juu yake. Kichwani alifunga kilemba.” Hii inatupa picha halisi ya huyo kaka kwani tunaposoma ni kama kweli tunamuona kutokana na jinsi mwandishi alivyoelezea. Pia uk.135 “mwambie yule jamaa pale atayarishe kuku mzuri wa kukaanga”……… na kachumbari yenye pilipili” hii inamfanya msomaji ahisi ladha ya kuku na hiyo pilipili kwa maneno ambayo mwandishi ameyajengea taswira na hii ni taswira hisi.
  • la mdimu ni taswira ya nyoka mbaya ambaye amefananishwa na viongozi wabaya.

WAHUSIKA
AMANI
  • Ni dereva taxi
  • Ana upendo wa dhati
  • Ni mchapakazi
  • Ana hekima na busara
  • Ana huruma
  • Ni rafiki wa kweli wa Tino
  • Kutokana na hizo sifa amani ni mhusika bapa
  • Anafaa kuigwa na jamii
TINO (mhusika bapa)
  • Ni mchapakzi
  • Mlezi bora wa familia
  • Baba wa Cheche
  • Ana huruma
  • Ana upendo wa dhati
  • Ni makini
  • Ni jasiri
  • Ni mwanamichezo
  • Anafaa kuigwa na jamii
BROWN KWACHA
  • Ni mkurugenzi wa idara ya fedha za kigeni
  • Ni muhuni na Malaya
  • Fisadi na mla rushwa
  • Anafanya biashara haramu
  • Hana mapenzi kwa familia yake
  • Anapenda anasa
  • Si muaminifu kwa mkewe
  • Si muadilifu
  • Hafai kuigwa na jamii
  • Ni mhusika bapa
JINJA MALONI
  • Ni jasiri na mwenye nguvu
  • Ana huruma na upendo
  • Mchapakzi
  • Mlevi
  • Maskini
  • Ni mhusika duara
DAKTARI MIKWALA
  • Ni daktari bingwa wa mifupa
  • Anapenda rushwa
  • Si muwajibikaji katika kazi yake
  • Ni mlevi
  • Hafai kuigwa na jamii
  • Ni mhusika bapa
SHIRAZ BHANJ
  • Ni mfanyabiashara
  • Ni mtoa rushwa
  • Ana biashara za magendo
  • Rafiki wa Brown
  • Hafai kuigwa na jamii
  • Ni mhusika bapa
ZITTO
  • Ni mfanyakazi bandarini
  • Ni mwanamichezo
  • Ni jasiri ana kipato duni
  • Rafiki wa Tino na Amani
CHECHE
  • Ni mtoto wa Tino
  • Ana nidhamu na bidii
  • Ni mwanamichezo
  • Ana upendo kwa wazazi wake
  • Ni mtiifu na msikivu
  • Mcheshi na mudadisi
  • Alivunjika kiuno michezoni
  • Ni mhusika bapa
MWEMA
  • Ni mke wa Tino
  • Mvumilivu
  • Ana mapendo ya dhati kwa familia yake
  • Ni mchapakazi
  • Ni mhusika bapa
JOSEPHINE NA LEILA
  • Wasichana wahuni waliojiuza kwa Brown Kwacha
  • Hawafai kuigwa na jamii

MANDHARI
Mandhari aliyoitumia mwandishi ni ya mjini, anataja baadhi ya maeneo ya nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kama vile Boko, Sega, Mindule. Mandhari hii ni sadifu kwa yale ambayo mwandishi ameyaeleza kwani masuala ya rushwa, upotevu wa haki, hali ngumu ya uchumi na maisha kwa ujumla, ni matatizo halisi ya jamii ya Tanzania.

www.CodeNirvana.in

Inaendeshwa na Blogger.

Translate

Total Pageviews

Copyright © tunda | Designed By Code Nirvana